Kila siku, binadamu anafanya maamuzi takriban 35,000. Kuanzia kitu gani ule asubuhi, hadi maamuzi mazito ya biashara au mahusiano. Lakini, je, umewahi kujiuliza kwa nini wakati mwingine unafanya maamuzi ya kijinga hata kama unajua kabisa siyo sahihi na unapoyakumbuka huwa unabaki kujicheka mwenyewe?
Shida siyo uwezo wako wa kufikiri; shida ni kwamba ubongo wako una "mifumo ya siri" ambayo usipoielewa, itakuongoza shimoni. Ili ufanikiwe, lazima ujifunze jinsi ya "kuendesha" akili yako badala ya kuiacha ikuendeshe.
Hizi hapa ni siri 5 ambazo hukuzijua, zitakazokufanya uwe mtaalamu wa kufanya maamuzi sahihi.
1. Ubongo Una 'Mifumo Miwili' Ya Maamuzi (System 1 & System 2)
Mwanasaikolojia Daniel Kahneman aligundua kuwa ubongo una gia mbili:
System 1 (Gia ya Haraka): Hii ni ya hisia, silika, na haraka. Inafanya kazi bila wewe kufikiria (kama kukwepa gari).
System 2 (Gia ya Polepole): Hii ni ya mantiki, uchambuzi, na nguvu. Inatumia nishati nyingi.Siri ni kwamba binadamu wengi wanafanya maamuzi ya maisha (kama kuoa au kuwekeza pesa) kwa kutumia System 1 (hisia za haraka) badala ya System 2.
Ufafanuzi wa Kina: Unapofanya uamuzi ukiwa na hasira, furaha sana, au hofu, unatumia System 1. Genius anajua wakati wa "kupunguza gia" na kulazimisha System 2 iingie kazini. Kabla ya kutoa jibu la uamuzi mkubwa, jipe dakika 10 au lala kwanza. Hii inaruhusu akili ya uchambuzi kuchukua hatamu.
2. 'Decision Fatigue': Ubongo Wako Unachoka Kama Msuli
Je, umewahi kugundua kuwa jioni unakuwa na tabia ya kufanya maamuzi mabaya? Labda ndiyo wakati unakula chakula cha ovyo au unatumia pesa vibaya. Hii inaitwa Decision Fatigue.
Kila uamuzi unaofanya, hata uwe mdogo kiasi gani, unatumia "betri" ya akili yako. Inapofika jioni, betri inakuwa imebaki 1%, na ubongo unatafuta njia rahisi zaidi (shortcut), ambayo mara nyingi siyo sahihi.
Ufafanuzi wa Kina: Watu kama Mark Zuckerberg au marehemu Steve Jobs walikuwa wanavaa nguo za aina moja kila siku ili wasipoteze nishati ya akili kufanya uamuzi wa "nivae nini?". Hifadhi maamuzi yako mazito kwa ajili ya asubuhi wakati betri yako iko 100%. Usifanye uamuzi wa mamilioni saa kumi na moja jioni ukiwa umechoka.
3. Mtego wa 'Loss Aversion': Hofu Ya Kupoteza Inakufanya Uwe Mwoga
Ubongo wa binadamu umeumbwa kuogopa kupoteza kitu mara mbili zaidi ya unavyofurahia kupata kitu. Hii inaitwa Loss Aversion. Hii ndiyo sababu unaweza kubaki kwenye kazi unayoichukia au biashara inayofeli kwa sababu tu unaogopa "kupoteza" kile ulichonacho, hata kama mbele kuna fursa kubwa zaidi.
Ufafanuzi wa Kina: Ili kufanya uamuzi sahihi, jiulize: "Je, ningekuwa sina hii nafasi leo, ningeipigania kuipata?" Kama jibu ni hapana, basi unaing'ang'ania kwa hofu tu, siyo kwa faida. Mageneus wanafanya maamuzi kwa kuangalia faida ya mbeleni, siyo kwa kuogopa hasara ya sasa.
4. 'Confirmation Bias': Ubongo Wako Unapenda Kusikia Unachokijua
Hii ni siri hatari sana. Ubongo wako hautaki kukosolewa. Unapokuwa na wazo, akili yako itatafuta taarifa zote zinazounga mkono wazo hilo na itazipuuza taarifa zote zinazosema unakosea. Hii ndiyo sababu watu wanabaki kwenye imani potofu hata kama ukweli uko wazi.
Ufafanuzi wa Kina: Mtaalamu wa maamuzi hutafuta watu wanaompinga. Kabla ya kufanya uamuzi mkubwa, tafuta mtu unayemwamini na mwambie: "Nipinge, nionyeshe wapi nakosea." Ukishinda hoja za wanaokupinga, hapo ndipo unapokuwa na uamuzi imara.
5. Siri ya 'Gut Feeling' (Silika): Sikiliza Ubongo Wako Wa Pili
Hii inaonekana kama haina mantiki, lakini ina sayansi nzito. 'Gut feeling' yako ni matokeo ya maelfu ya kumbukumbu na mifumo ambayo ubongo wako umeihifadhi bila wewe kujua. Wakati mwingine akili yako inajua jibu kabla hujapata muda wa kulichambua.
Ufafanuzi wa Kina: Hata hivyo, usitumie silika pekee. Kanuni bora ni: Tumia mantiki (System 2) kukusanya taarifa, kisha tumia silika (Gut feeling) kufanya maamuzi ya mwisho. Kama kila kitu kwenye karatasi kinaonekana sawa lakini "moyo" unadunda kwa wasiwasi, simama kwanza. Ubongo wako wa ndani unaweza kuwa umeona kitu ambacho macho yako hayajakiona.
Hitimisho: Kuwa Dereva Wa Akili Yako
Kufanya maamuzi sahihi siyo kipaji, ni mfumo. Ukielewa kuwa ubongo unachoka, unaogopa hasara, na unajidanganya wenyewe, unakuwa umepata funguo za ushindi.
Kuanzia leo, usikimbilie kutoa jibu. Pima: Je, ni hisia au mantiki? Je, nimechoka? Je, naogopa kupoteza?Usikurupuke kamwe katika kufanya maamuzi hasa katika nyakati ngumu maana ndio huwa zinaamua hatma ya maisha yako eidha zikunyayue au zikumwage.Tukutane kwenye makala nyingine karibu sana E-ONLINE MAKALA.




